Jumanne 27 Oktoba 2026 - 18:00
Tume ya Haki za Binadamu ya Yemen Yalaani Vikali Shambulio la Saudi Arabia Dhidi ya Hospitali ya Wazazi na Watoto Huko Taiz

Hawza/ Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Yemen imelitaja shambulio la moja kwa moja lililofanywa na ndege za kivita za Saudi Arabia dhidi ya Hospitali ya Wazazi na Watoto katika Wilaya ya Al-Shamaytayn, Mkoa wa Taiz, kuwa ni uhalifu kamili wa kivita.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Yemen imelaani vikali kulengwa moja kwa moja Hospitali ya Wazazi katika Wilaya ya Al-Shamaytayn, iliyoko Mkoa wa Taiz, na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia.

Katika taarifa yake, tume hiyo ilisema: “Katika uhalifu mpya wa kivita unaoongezwa kwenye historia chafu iliyojaa damu ya wananchi wa Yemen, ndege za kivita za adui wa Saudi Arabia ziliilenga Hospitali ya wakina mama na watoto katika Wilaya ya Al-Shamaytayn, Mkoa wa Taiz, moja kwa moja na kwa makusudi.”

Taarifa hiyo ilieleza kuwa shambulio hilo lilisababisha uharibifu mkubwa katika sehemu muhimu za hospitali hiyo, zikiwemo wodi ya watoto wachanga, wodi ya wazazi na kitengo cha dharura, na hatimaye kuifanya hospitali hiyo isimamishe kabisa huduma zake. Haya yalitokea wakati hospitali hiyo ikiwa imejaa wanawake wajawazito, watoto wachanga waliokuwa wakinyonya na watoto waliozaliwa muda mfupi uliopita.

Tume ya Haki za Binadamu ilisisitiza kuwa kuishambulia taasisi ya afya ambayo inalindwa chini ya Sheria ya Kimataifa ya Kibinadamu, hususan hospitali maalumu kwa ajili ya kinamama na watoto, halikuwa kosa la kijeshi wala kulenga shabaha kimakosa. Badala yake, ilisema kuwa lilikuwa ni tendo la kihalifu lililoamuliwa na kupangwa kimakusudi, na hivyo kuwa uhalifu kamili wa kivita kwa mujibu wa Kifungu cha 18 cha Mkataba wa Nne wa Geneva na Kifungu cha 12 cha Itifaki ya Ziada ya Kwanza, ambavyo vinaharamisha mashambulizi ya mabomu dhidi ya hospitali na vitengo vya matibabu.

Tume hiyo iliuliza: “Adui wa Saudi Arabia anataka nini kutoka kwa mtoto mchanga aliye ndani ya mashine ya kumtunzia mtoto mchanga (incubator) na mama aliye kwenye kitanda cha kujifungulia? Ni mpango gani mchafu wa kijeshi unaofanya mwanamke na sauti ya kilio cha mtoto wake mchanga kuwa shabaha ya ndege za kivita za F-16 na Typhoon?!”

Taarifa hiyo iliongeza kuwa, baada ya kushindwa kukabiliana na wapiganaji katika medani za mapambano ya heshima na ushujaa huko Saada, maeneo ya mpakani, Al-Jawf, Pwani ya Magharibi na maeneo mengine, adui wa Saudi Arabia ameamua kumwaga chuki na uchungu wa kushindwa kwake kwa kuwalenga akina mama na miili ya watoto.

Tume ya Haki za Binadamu iliitaja serikali ya Saudi Arabia, pamoja na nchi zote zinazoiuzia silaha na risasi na zile zinazoiunga mkono  kisiasa, yaani serikali za Marekani na Uingereza, kuwa zinawajibika kikamilifu kisheria na kwa makosa ya jinai kutokana na uhalifu huo.

Aidha, tume hiyo ilieleza kushangazwa kwake na ukimya wa Umoja wa Mataifa, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF). Ikizielekezea taasisi hizo ujumbe wake, ilisema: “Inatosha sasa ukimya… Inatosha sasa kushirikiana katika kuficha uhalifu… Mlikuwa kimya walipolenga shule; mlikuwa kimya waliposhambulia masoko, viwanda na mashamba; na leo hii hospitali ya wazazi imelengwa. Kesho itakuwa nini?”

Taarifa hiyo iliendelea kusema: “Ukimya wenu hauwezi tena kuitwa kutokuwa na upande wowote, bali ni kushiriki katika uhalifu. Taarifa zenu za kueleza wasiwasi hazina hata thamani ya gesi na pamba iliyolowa damu za akina mama huko Al-Shamaytayn.”

Tume ya Haki za Binadamu ilisisitiza kuwa Yemen inahifadhi haki yake ya kuwafungulia mashtaka na kuwafuatilia viongozi wa upande unaofanya mashambulizi hayo katika mahakama za kimataifa kama wahalifu wa kivita. Pia, ilisisitiza kuwa uhalifu huu hautafutika kwa kupita muda.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha